NA WILLIUM PAUL, SAME.
KATIBU wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), katika Jimbo la Same magharibi, Aika Ngowi amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwateuwa viongozi bora ambao wamekuwa mstari wa mbele kuwaunganisha wananchi bila kujali itikadi za vyama pamoja na kutatua kwa vitendo kero za Wananchi.
Katibu huyo alitoa kauli hiyo jana wakati walipoalikwa na Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni katika Iftar aliyoiandaa nyumbani kwake iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya siasa na waumini wa madhehebu ya kiislam na kikristo.
Aika alisema kuwa, viongozi walioteuliwa na Rais kuhudumu katika wilaya ya Same wameonyesha utendaji kazi kwa vitendo ikiwemo kushuka kwa wananchi na kusikiliza kero zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi na kudai kuwa chama chao ndivyo kinavyotaka kuona wananchi wakihudumiwa kwa vitendo.
“Mkuu wa wilaya tunatambua utendaji wako wa kazi na tunakuomba uendelee hivo hivo umekuwa kiongozi wa mfano na wa kuigwa katika kutuunganisha Wananchi wa Same pamoja na juhudi zako za kutatua changamoto za wananchi kupitia kliniki iliyoianzisha ya kero hiki sisi kama Chadema ndicho tunachokitaka nimpongeze Rais Dkt. Samia kwa kukuteuwa kuja Same” alisema Aika.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya Kasilda Mgeni, amewasihi viongozi wa dini pamoja na waumini wa dini mbalimbali kutumia kipindi cha mfungo kuliombea Taifa la Tanzania na kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kuliongoza vyema Taifa huku akieleza mafanikio ya maendeleo yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika sekta mbalimbali.
Kasilda alisema lengo la iftar hiyo ni kujumuika pamoja na kutumia nafasi hiyo kuombea Taifa na viongozi wake ili Tanzania izidi kuwa na amani, utulivu, pamoja na ustawi wa uchumi na maendeleo.
“Niwaombe sana viongozi wa dini na waumini wa dini mbalimbali mliojumuika nasi kwenye iftar hii, tunapoendelea na funga zetu tutumie sana kipindi hiki kuliombea kheri Taifa letu na kiongozi wetu mpendwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kuliongoza vyema Taifa letu kama tunavyoshuhudia, mambo makubwa yanaendelea kufanyika hapa nchini, na Wilaya ya Same ni miongoni mwa wanufaika wakubwa,” alisema Kasilda.
Sheikh wa Wilaya ya Same, Sheikh Iddi Ally, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuandaa iftar hiyo iliyowaunganisha viongozi wa dini mbalimbali, taasisi za serikali na binafsi, wadau wa maendeleo, vyama vya siasa pamoja na wananchi kusisitiza umuhimu wa waumini wa dinizote kuendelea kumuombea dua Rais.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Same, Abdallah Mnyambo, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda amani iliyopo bila kujali itikadi za dini, siasa, au hali za kiuchumi.
Aidha Kasilda alitumia nafasi hiyo kubainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wilaya ya Same imepokea kiasi cha shilingi bilioni 380.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.