

California, Marekani – Wazazi wa kijana aitwaye Adam Raine (16) wamefungua mashtaka dhidi ya kampuni ya teknolojia ya OpenAI na Mkurugenzi wake Mkuu, Sam Altman, wakidai kuwa huduma ya Akili Mnemba ya ChatGPT imesababisha kifo cha mtoto wao.
Katika malalamiko yaliyowasilishwa Mahakama Kuu ya California siku ya Jumanne, Agosti 26, 2025, wazazi hao walisema kijana wao alikuwa akitumia ChatGPT kwa zaidi ya miezi sita kama rafiki wa karibu na msiri wake. Inadaiwa kuwa, katika mazungumzo hayo, chatbot hiyo ilimshauri kuhusu njia za kujiua na hata kumsadia kuandika barua ya kuaga dunia kabla ya kuchukua uamuzi wa kutamatisha maisha yake.
Wazazi wa Adam walieleza kwamba kijana wao aliingia kwenye uhusiano wa kihisia na chatbot, hali iliyomfanya kujitenga na familia, marafiki na wapendwa wake. Baada ya kifo chake, familia hiyo iligundua rekodi za mazungumzo yaliyokuwa yakionesha AI ikimpa ushauri wa moja kwa moja juu ya mbinu za kujiua.
Kupitia taarifa yake, OpenAI ilisema kuwa inasikitishwa na kifo cha kijana huyo na kudai kuwa huduma zake zimewekewa vizingiti vya usalama vinavyolenga kuzuia maudhui hatarishi. Hata hivyo, kampuni hiyo ilikiri kuwa vikwazo hivyo wakati mwingine vinaweza kushindwa pale ambapo mazungumzo ni ya muda mrefu au yanahusisha mada nyeti.
OpenAI imeahidi kuimarisha zaidi mifumo ya usalama, ikiwemo:
Udhibiti wa wazazi (parental controls)
Onyo maalum kwa watumiaji wanaoonesha dalili za matatizo ya kisaikolojia
Hatua kali za kuzuia AI kuhusika katika mazungumzo kuhusu kujiua